Tiketi Za Treni Kununuliwa Kwa Njia Ya Mfumo Wa Kielektroniki..!!

Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) inatarajia kuanza kutoa huduma ya uuzaji wa tiketi kwa abiria wanaotumia usafiri wa treni kwa mfumo wa kielektroniki lengo likiwa ni kuwawezesha wananchi kuweza kurahisha ununuaji wa tiketi hizo na kupunguza usumbufu.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Profesa Makame Mbarawa wakati akijibu swali la nyongeza lililoihusu Wizara yake ambapo ametaja maeneo ambayo mfumo huo utaanza kufanya kazi ni pamoja na Mpanda mpaka Tabora, Kigoma mpaka Tabora.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Mhandisi Edwin Ngonyani akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Sabreen Hamza lililotaka kujua kwanini TRL isianzishe mfumo wa uwakala wa tiketi ili kupunguza adha wanayoipata wakazi alisema kuwa kutokana na mahitaji makubwa ya usafiri wa treni katika Mikoa ya Kigoma, uuzaji wa tiketi katika Stesheni ya Reli Kigoma umekuwa na changamoto kubwa kutokana na ulanguzi wa tiketi.

Amefafanua kuwa, ili kudhibiti ulanguzi huo, Kampuni ya Reli Tanzania iliamua kubadilisha utaratibu kwa kuuza tiketi siku za safari na kwa kutumia vitambulisho jambo ambalo limesaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti ulanguzi wa tiketi hizo.

Ameongeza kuwa, utaratibu huo umekuwa na changamoto zake kwa kusababisha wasafiri kulala stesheni au kuwalazimu kuamka alfajiri ili kuwahi tiketi hizo.

"Ufumbuzi wa kudumu wa tatizo hili si kuanzisha mfumo wa uwakala ambao utaiongezea TRL gharama za uendeshaji, tatizo kubwa lililopo ni idadi ndogo ya safari za treni ambapo huduma inayotolewa hivi sasa haikidhi mahitaji halisi ya wananchi na hivyo kuwa na uhaba wa tiketi kwa abiria", alisema Mhe. Ngonyani.

Aliongeza kuwa ili kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali inatarajia kuongeza idadi ya treni za abiria kwa njia ya Kigoma ili kukidhi mahitaji ya wananchi wa Mkoa huo.

Comments

Popular posts from this blog

ZINGATIA HAYA UKITAKA KURUDIANA NA MPENZI WAKO WA ZAMANI

Waziri Mkuu Ashangazwa Na Kodi Kubwa Soko La Dodoma.....Aagiza Baraza La Madiwani Lipitie Upya Na Kumpa Majibu

ALAMA YA NYOKA KWENYE NEMBO MBALIMBALI INA MAANA KUBWA