Lowassa Azidi Kuipasua CCM



Uamuzi wa Edward Lowassa kujiondoa CCM na kujiunga Chadema, bado unakitesa chama hicho tawala baada ya mikoa kuanza kuwashughulikia viongozi waliomuunga mkono wakati wa Uchaguzi Mkuu, huku baadhi wakisema wako tayari kupambana na wanaowatuhumu kusaliti chama.

Lowassa alijiengua CCM Julai mwaka jana baada ya jina lake kuondolewa kwenye mbio za urais kwa tiketi ya chama hicho, na baadaye kufuatwa na mawaziri, wabunge, wenyeviti wa mikoa na madiwani na hivyo kufanya Uchaguzi Mkuu kuwa na ushindani mkubwa.

Baada ya kumalizika kwa uchaguzi huo, viongozi na wanachama wa CCM walioonekana kuwa karibu na waziri huyo mkuu wa zamani, walituhumiwa kukihujumu chama kwa kumpigia kampeni Lowassa wakati wa usiku, huku mchana wakijionyesha kuwa wanaunga mkono wagombea wa CCM.

Tuhuma hizo ziliongezewa nguvu na mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete takriban wiki mbili zilizopita alipotangazakuwa waliosaliti chama hicho watatumbuliwa bila ya aibu, na tayari mkoa wa Manyara umeshatangaza kuwatimua uanachama viongozi 21 wanaotuhumiwa kushabikia upinzani.

Viongozi wa mikoa  wamekanusha tuhuma zinazoelekezwa kwao kuwa walisaidia upinzani wakati wa uchaguzi wa mwaka jana.

Miongoni mwa wanaotuhumiwa ni mwenyekiti wa Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu ambaye aliangushwa kwenye kura za maoni ndani ya chama hicho na Frederick Mwakalebela, ambaye pia alishindwa na Mchungaji Peter Msigwa kwenye kinyang’anyiro cha ubunge wa Jimbo la Iringa Mjini.

Mwenyekiti huyo anatuhumiwa kubadili timu yake ya kampeni na kuifanya iwe ya kumpigia debe mgombea huyo wa Chadema.

Lakini Msambatavangu, ambaye pia anadaiwa kutoa gari zake zitumike kwenye kampeni za wapinzani, alisema yupo tayari kuhojiwa ili ajibu tuhuma dhidi yake ambazo tayari zimewasilishwa kwenye chama hicho.

Alisema anasubiri ahojiwe ili aeleze ukweli kuhusu suala hilo.
Mwakalebela alifungua kesi Mahakama Kuu akidai kuwa taratibu zilikiukwa wakati wa kuhesabu kura.

Mwingine anayezungumzwa ni mwenyekiti wa CCM wa Simiyu, Dk Titus Kamani, ambaye alikuwa Waziri wa Uvuvi na Maendeleo ya Mifugo katika Serikali iliyopita, ambaye amezielezea tuhuma dhidi yake kuwa ni majungu ya wasiompenda ambao wanataka avuliwe uongozi.

Dk Kamani anadaiwa kuwawezesha kwa hali na mali baadhi ya wagombea wa upinzani, kama kutoa vyombo vya matangazo na gari lake wakati wa kampeni.

Comments

Popular posts from this blog

DC AWAAGIZA WALIOVAMIA EPZA WAONDOKE.

ALAMA YA NYOKA KWENYE NEMBO MBALIMBALI INA MAANA KUBWA

Makala : Fahamu Kuhusu Ndumba Za Kichawi Na Jinsi Ya Kujikinga Nazo.