WAKAMATWA NA MAGAMBA YA KAKAKUONA

WATU wanne wakiwemo raia watatu wa Burundi, wanashikiliwa na Polisi mkoani Morogoro baada ya kukutwa na magamba ya kakakuona, yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 1.4.

Walikuwa wamehifadhi magamba hayo kwenye mifuko 67, yakisubiri kusafirishwa kwenda nje ya nchi kuuzwa. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei, alisema watu hao walikamatwa saa tano na nusu usiku wa Oktoba 28, mwaka huu eneo la mtaa wa Reli, kata ya Kichangani, Manispaa ya Morogoro.

kakakuona

Walinaswa ndani ya ghala moja, lenye mashine ya kukoboa na kusaga nafaka.

Alisema, askari wa jeshi hilo wakiwa katika msako, walipokea taarifa za kiintelejensia kutoka kwa raia wema kuhusu mazingira ya watu katika eneo hilo. Walipofika, walikuta watuhumiwa hao wanne.

Baada ya upekuzi kwenye ghala hilo, polisi walikamata magamba ya kakakuona katika mifuko 67, baaadhi yake yakiwa tayari kwa ajili ya kusafirishwa kwenda nje ya nchi.

Kamanda Matei aliwataja raia wa Burundi waliokamatwa kuwa ni Kibonese Golagoza ( 35), Nuru Athuman (32) na Benjamin Gregory Luvunduka (41) ambao pia ni wakazi wa Morogoro, wakati Mtanzania ni Shukuru Mwakalebela (25) mkazi wa Stesheni mjini hapa.

Alisema magamba hayo, yalifungwa katika mifuko yenye kilo 50 na kisha kutumbukizwa kwenye viroba vikubwa vya kilo 100, vilivyochanganywa na maharage. Aidha alisema watuhumiwa raia wa Burundi, wanakabiliwa pia na tuhuma za kuingia nchini bila kibali cha Uhamiaji.

Ofisa Maliasili wa Mkoa wa Morogoro, Joseph Chuwa aliyekuwepo katika upekuzi huo, alisema katika mifuko 67 iliyokamatwa, kila mmoja ulikuwa na wastani wa magamba ya kakakuona 1,000.

Alisema kakakuona mmoja, kwa wastani anakuwa na magamba 60 hadi 100, hatua iliyofanya kila mfuko kuwa na wastani wa kakakuona wapatao 10 waliouawa kwa ajili ya biashara hiyo haramu.

Alisema kutokana na idadi ya mifuko hiyo, wastani wa kakakuona 670 waliuawa, ambapo kilo moja ya magamba yake huuzwa kwa dola za Marekani 960, hivyo kutokana na viwango vya sasa vya thamani ya dola kwa fedha ya Tanzania, ni sawa na Sh bilioni 1.4.

Comments

Popular posts from this blog

ZINGATIA HAYA UKITAKA KURUDIANA NA MPENZI WAKO WA ZAMANI

ALAMA YA NYOKA KWENYE NEMBO MBALIMBALI INA MAANA KUBWA

IPI ZAWADI SAHIHI KWA MAHARUSI?