Lowassa afunguka mengi Leo....Adai hakuna mwenye hati miliki Ya Nchi
Waziri Mkuu Mstaafu na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowasa amemtaka Rais John Magufuli kuwa na utamaduni wa kufanya mazungumzo na wanasiasa wenzake ili kufikia muafaka wa mambo mbali mbali ya kisiasa nchini.
Lowasa ameyasema hayo leo wakati wa mahojiano na Tido Mhando kupitia kipindi cha Funguka kinachorushwa na Televisheni ya Azam. Lowasa amesema kuwa siasa ni mazungumzo na siyo kutoa tu amri kama anavyofanya Rais Magufuli.
Kadhalika Lowassa amesema kila mtu ana wajibu wa kuheshimu amani ya nchi na hakuna mtu mwenye hati miliki ya nchi hii.
“Serikali haipaswi kuwa na ghadhabu, inapaswa kuwa na tabia ya kuzungumza. Sisi sote ni Watanzania kwa nini tunaogopa kuzungumza. Mazungumzo ndiyo njia bora ya kufikia maridhiano. Pia Rais Magufuli aitazame Zanzibar, tunasikia watu wanashughulikiwa kwa njia mbalimbali, wanakamatwa, hivyo hawezi kuikwepa Zanzibar kwani hilo ni suala lake.” alisema Lowassa.
Amesema CHADEMA ipo sahihi kutangaza operesheni ‘Ukuta’ hapo Septemba 1, mwaka huu na kwamba bado kuna nafasi ya kufanya mazungumzo kabla ya tarehe hiyo kufika ili kuepusha hali ya migogoro itakayojitokeza siku hiyo itakapofika.
Akizungumzia barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa kukemea operesheni hiyo, amesema barua hiyo imejaa ghadhabu zaidi kuliko kuongelea mambo ya msingi ambayo vyama vya upinzani vimekuwa vikionewa.
Akiongelea suala la wabunge wa upinzani kutoka na kususia bunge, Lowassa amesema hali hiyo ilisababishwa na kutokuwepo kwa Spika Job Ndugai ambaye kwa muda mrefu alikuwa nje ya nchi akiendelea na matibabu.
“Ndugai angekuwepo haya yote yasingetokea kwakuwa ni mtu makini sana na hata kwa Naibu Spika kuna tatizo la Kisaikolojia kwasababu aliingia bungeni kwa njia zisizoeleweka na hivyo kumfanya kushindwa kuhimili kiti vizuri,” amesema.
Hata hivyo amempongeza Rais Magufuli na kudai kuwa amefanya vizuri katika baadhi ya maeneo lakini kuna maeneo mengine ambayo angepaswa kuyapa kipaumbele zaidi akitolea mfano wa elimu na kudai kuwa badala ya kuanza na suala la madawati angeanza na kushughulikia maslahi ya walimu kwanza, na kutoa kipaumbele kwa tatizo la ajira nchini hasa kwa vijana.
Kuhusiana na harakati za Serikali kuhamia Dodoma, Mjumbe huyo wa Kamati Kuu CHADEMA amesema viongozi wote waliotangulia tangu enzi za Mwalimu Nyerere walikuwa na ndoto za kuhamia Dodoma lakini kuna mambo yaliyokuwa yanaingilia mipango hiyo na mwisho kushindikana.
“Napongeza harakati na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuhamishia Serikali yote Dodoma lakini napenda kuwaambia wasiende kwa kasi sana wasije wakavunjika miguu,” ameongeza.
Kuhusiana na hali ya kisiasa Zanzibar, Lowassa ametoa rai kwa Rais Magufuli aangalie hali ya Zanzibar kwani yanayoripotiwa kuendelea visiwani humo yanatia kichefuchefu ikiwemo watu kukamatwa na kuteswa.
“Tusiitenge Zanzibar na badala yake juhudi za makusudi zifanyike kuweka mambo sawa kwa kufanya mazungumzo kwani siasa ni mazungumzo,” amesisitiza Lowassa ambaye amedai kuwa ana matumaini makubwa ya kuingia Ikulu mwaka 2020.
Kuhusu kashfa ya Richmond kumfanya aondoke CCM kwa hasira baada ya kukosa ridhaa ya chama hicho katika kugombea Urais, Lowassa amesema hakuondoka CCM kwa hasira isipokuwa alituhumiwa na kuhukumiwa bila kupewa nafasi ya kusikilizwa.
“CHADEMA sikujipeleka mwenyewe bali Kamati Kuu CHADEMA ilinifata na kuniomba nijiunge nao katika kupeperusha bendera yao na mimi niliona ni ‘opportunity’ nzuri hivyo nikakubali nikajiunga nao na tukafanikiwa kupata kura zaidi ya milioni sita, idadi ambayo siyo ndogo hata kidogo,” amejinasibu Lowassa.
Comments
Post a Comment