Halima Mdee na Ester Bulaya Kulipwa nusu mshahara kwa miezi 10 nje ya Bunge
Wabunge wa Chadema, Halima Mdee (Kawe) na Ester Bulaya (Bunda Mjini) ambao wamesimamishwa kuhudhuria vikao vya Bunge, watalipwa nusu mshahara na posho zinazoambatana nao kwa miezi kumi.
Stahiki hizo ni kwa mujibu wa kanuni ya 75 ya Bunge inayosema, “mbunge aliyesimamishwa hataingia tena sehemu yoyote ya ukumbi na maeneo ya Bunge kwa muda wote atakapokuwa amesimamishwa na atalipwa nusu mshahara na nusu posho zinazoambatana na mshahara huo.”
Vilevile, kutokana na uamuzi huo wabunge hao watakosa siku 65 za Bunge zinazojumuisha siku 25 zilizobaki za Bunge la bajeti linaloendelea, Bunge la Oktoba na lile la Februari, 2018. Vikao vya mabunge hayo mawili; la Oktoba na Februari kila kimoja huwa na mikutano ya wiki mbili mbili.
Wabunge hao walisimamishwa juzi kwa azimio la Bunge licha ya kutokuwapo au kujitetea kutokana na tuhuma zilizokuwa zinawakabili za kudharau kiti cha spika.
“Tukutane Bunge lijalo la bajeti,” alisema juzi Spika wa Bunge, Job Ndugai. Bunge la bajeti huanza mwezi Aprili.
Kufikia uamuzi huo, kamati ya haki, maadili na madaraka ya Bunge ilisema iliwatafuta kwa simu wabunge hao, lakini haikuwapata. Pia, iliwatumia ujumbe mfupi ambao haukujibiwa na ilipowapelekea hati ya wito haikuwakuta majumbani kwao.
Kwa kutambua umuhimu wa agizo ililonalo na kuzingatia matakwa ya kisheria, hati hizo ziliachwa baada ya kuelezwa kwamba wahusika hawapo kwani wamesafiri. Baada ya jitihada hizo kushindwa kuzaa matunda, kamati iliendelea kuwajadili bila wao kuwapo na kutoa maazimio hayo.
Comments
Post a Comment