Kivuko Kipya kilichozinduliwa na kukabidhiwa kwa Waziri Mbarawa

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amepokea Kivuko cha MV Kazi kutoka kwa Kampuni ya kizalendo ya M/S Songoro Marine Transport Boatyard ya Mwanza iliyokuwa inafanya kazi ya ujenzi wa Kivuko hicho mara baada ya ujenzi wake kukamilika.

Akizungumza na wananchi, Prof Mbarawa jana alisema lengo la Serikali kuongeza Kivuko hicho  ni kuboresha huduma za kusafirisha abiria na magari kati ya Magogoni na Kigamboni.

“Uwepo wa vivuko vitatu kutasaidia utoaji wa huduma kwa wakati na kwa urahisi na ikitokea Kivuko kimoja kimepelekwa kufanyiwa ukarabati huduma zitaendelea kama kawaida bila kuathiri utaratibu wa kawaida”.Alisema Prof Mbarawa.

Aliongeza kuwa ili kuendana na kasi ya Mhe. Rais John Magufuli  Wizara yake itaendelea kuboresha huduma za Vivuko katika Mikoa mingine ikiwemo Mkoa wa Lindi , Kivuko cha Pangani, na Kivuko cha Kigongo Busisi Mkoani Mwanza.

Nae Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Dkt. Dkt. Mussa Mgwatu alisema Kivuko cha MV Kazi kimejengwa kulingana na viwango vinavyotakiwa Kimataifa na ukaguzi wake umefanywa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) na kuthibitishwa kuwa ni salama kwa ubebaji wa abiria na magari.

 Ujenzi wa MV KAZI umegharimu Shilingi Bilioni 7.3 za Kitanzania na kina uwezo wa kubeba abiria 800 magari 22 sawa na jumla ya tani 170.

Kivuko hicho kimekabidhiwa jana  kwa ajili ya kuanza kutoa huduma kati ya Magogoni na Kigamboni Jijini Dar es salaam na kuongeza idadi ya vivuko katika eneo hilo kufikia vitatu.



Comments

Popular posts from this blog

ZINGATIA HAYA UKITAKA KURUDIANA NA MPENZI WAKO WA ZAMANI

Waziri Mkuu Ashangazwa Na Kodi Kubwa Soko La Dodoma.....Aagiza Baraza La Madiwani Lipitie Upya Na Kumpa Majibu

ALAMA YA NYOKA KWENYE NEMBO MBALIMBALI INA MAANA KUBWA