Akamatwa kwa kumshawishi mpenzi wake ajiue kisha achangishe fedha mtandaoni
Msichana mwenye umri wa miaka 20, Michelle Carter atapandishwa kizimbani Massachusetts nchini Marekani wiki hii akikabiliwa na mashtaka ya kumshawishi mpenzi wake kujiua.
Carter anadaiwa kumshawishi kwa njia ya simu mara kadhaa aliyekuwa mpenzi wake, Conrad Roy III aliyefikia uamuzi wa kujiua kwa hewa ya ‘carbon monoxide’ miaka miwili na nusu iliyopita, ambapo mwili wake ulikutwa kwenye gari lake eneo la maegesho ya magari.
Upelelezi umeonesha kuwa msichana huyo alikuwa akimtumia jumbe za simu mpenzi wake huyo ambaye awali alimtaka Carter kumshauri baada ya kufanya jaribio ya kujiua bila mafanikio. Jumbe hizo zilimsihi marehemu kujiua tu huku zikimtia moyo kuchukua hatua hiyo.
Baada ya Conrad kujiua, mrembo huyo aliingia kwenye mtandao na kuanzisha kampeni ya kuchangisha fedha kwa lengo la kuwasaidia watu wenye matatizo ya kiakili akichukulia mfano wa uamuzi wa mpenzi wake huyo, hadi upelelezi ulipomuumbua na kumtia nguvuni.
Hata hivyo, mwanasheria wa Boston, Peter Elikann ameiambia CNN kuwa shauri hilo limewavutia wanasheria wengi kutaka kujua maamuzi ya mahakama yatakuwaje, maamuzi ambayo yanaweza kuchukuliwa kama chanzo cha sheria mpya kwani hadi sasa hakuna sheria inayoeleza juu ya tukio kama hilo.
“Hadi sasa hakuna sheria ya wazi kwenye vitabu vya Massachusetts kuhusu mtu kumshawishi mtu mwingine kujiua au kuacha kujiua,” alisema mwanasheria Elikann.
Wakati Carter anamshawishi mpenzi wake kuchukua uamuzi huo alikuwa na umri wa miaka 17 na miezi kadhaa na mpenzi wake huyo ambaye ni marehemu alikuwa na umri wa miaka 18.
Comments
Post a Comment