Mwandishi wa habari wa Kituo cha ITV mkoani Arusha, Khalfan Lihundi, anashikiliwa na polisi katika Kituo cha Polisi Usa River, wilayani Arumeru kwa tuhuma za kuandika habari zinazodaiwa kuwa ni za uchochezi. Lihundi alikamatwa jana jijini hapa majira ya saa nane mchana na askari anayedaiwa kutumwa na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti. Mmoja wa waandishi wa habari walioshuhudia tukio hilo, Basil Elias, alisema kuwa, walipokuwa ofisini, alifika ofisa wa polisi akidai ametumwa kumfuata Lihundi kwa ajili ya mahojiano. Kwa mujibu wa Elias ambaye alimnukuu ofisa huyo wa polisi, Lihundi anadaiwa kuandika habari ya uchochezi kuhusu mgogoro wa maji bila kumhoji mkuu huyo wa wilaya. “Habari hiyo inayodaiwa kuwa ni ya uchochezi, ilikuwa ni malalamiko ya wananchi juu ya tatizo la maji katika wilaya hiyo,” alisema Elias. Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari, Mkoa wa Arusha (APC), Claud Gwandu, pamoja na kulaani...